FAHAMU AINA 9 YA WATEJA KWENYE BIASHARA YAKO

Hawa ni wateja unazoweza kuzitumia kukuza biashara yako

1. Wateja wapya

2. Wateja watafutao punguzo

3. Wateja watiifu au wakudumu

4. Wateja mabalozi

5. Wateja watafiti

6. Wateja wapitaji

7. Wateja walalamikaji

8. Wateja wasiokuwa na mpango wa manunuzi

9. Wateja wanaotafuta ubora

Soma: Jinsi ya Kutengeneza Mpesa Mastercard

1. Wateja wapya

Mteja huyu huja kwa lengo la kupata huduma pamoja na  kuifahamu biashara husika ili kuona sababu itakayomfanya awe mteja wa biashara hiyo. Wewe kama mfanyabiashara, hutakiwi kufanya kosa kwa aina hii ya mteja; hakikisha mteja huyu anaifahamu biashara yako vyema na anapata sababu za kutosha za kuanza kuwa mteja wako wa kudumu. Unaweza kufanya haya yafuatayo kwa mteja huyu: Mpe maelezo kuhusu bidhaa au huduma unazotoa katika biashara yako, Mpe ofa ya ukaribisho, Onyesha sura na lugha nzuri itakayo mfanya aone ujio wake mpya umethaminiwa Ikiwa mteja huyu amehama kutoka kwenye biashara nyingine, basi dodosa ni sababu gani zimemfanya ahame. Mf. Utasikia mteja akisema “Kule kwenye lile duka fulani wanajisikia sana.”, “Yule muuzaji anauza vitu ghali sana.” n.k. Yachukue haya kama somo la kuboresha huduma yako.

2. Wateja watafutao punguzo

Hawa huja katika safari yao ya kutafuta punguzo la bei kwenye huduma au bidhaa wanayoitafuta. Mara nyingi wateja hawa wanaweza kutekwa na punguzo dogo sana ambalo hata wewe mwenyewe usingedhani kama linaweza kumshawishi mteja kununua huduma au bidhaa Jambo muhimu hapa inabidi ujue kucheza na bei za bidhaa vizuri, ni bora ukose hata shilingi hamsini au miamoja kwenye faida yako lakini uwapate wateja wa aina hii. Mf. kuna mteja anaweza kuacha kununua gesi kwenye duka inapouzwa shilingi 20,000 na kwenda kununua wanapouza 19,900.

3. Wateja watiifu au wakudumu

Hawa ndio wateja wakuu uliowazoea na waliokuzoea wewe. Ni wateja muhimu ambao wanapaswa kuthaminiwa na kuhudumiwa vyema.  Mara nyingi wateja hawa wanakuamini na wanaamini huduma na bidhaa ile unayoitoa.  Wateja hawa hawahamishwi kirahisi, Hawa Hupenda kutoa ushauri na mapendekezo kuhusu biashara na huduma kwa kuwa hujihisi kuwa nao ni sehemu ya biashara husika. Pia ni mabalozi wema wa biashara husika. Hupenda kuacha pesa zao kwako na kukopa. Hivyo basi, wewe kama mjasiriamali hakikisha unaongeza thamani ya huduma.

4. Wateja mabalozi

Wateja ambao ni mabalozi wanaweza wasiwe ni wateja wa mara kwa mara, lakini wakawa mabalozi wazuri au wabaya wa ile huduma au bidhaa unayouza. Wateja hawa hupenda kuwashirikisha watu wengine sifa za biashara yako ikiwa ni nzuri au ni mbaya. Wateja hawa huleta marafiki, majiran au hata wanafamilia wao kwenye biashara yako ikiwa wameridhishwa na huduma unayotoa. Ili kuhimiza wateja kuwa mabalozi:

• Toa huduma nzuri

• Toa ofa na punguzo

• Mshukuru mteja pale anapokuletea mteja mpya

• Tumia lugha nzuri itakayo kufanya uwe mfano

5. Wateja watafiti

Hii ni aina ya wateja ambao hufanya manunuzi baada ya kupata taarifa za kina kuhusu bidhaa au huduma ile wanayoitaka. 6. Wateja wapitaji Hawa ni wateja ambao huja kwenye biashara yako mara moja tu, na si rahisi kuja tena mara nyingine au karibuni. Mara nyingi wateja wa aina hii huwa ni wasafiri au watu walioletwa kwenye eneo lako la biashara kutokana na tukio fulani kama vile msiba au sherehe. Ingawa wateja hawa ni wapitaji, unapaswa kuwahudumia vyema kwani hujui kesho itakuwaje. Ili kuwapata wateja hawa ni vizuri kujenga jina jema katika eneo husika ili mteja mgeni afikapo katika eneo unalofanyia biashara akubaini wewe kwanza kabla ya kumbaini mfanyabiashara mwingine.

7. Wateja walalamikaji

HAWA wanapenda kulalamika na kulaumu sana. Si rahisi kuwaridhisha wateja hawa kwani wao kila kitu kwao ni tatizo. Hata hivyo, pamoja na tabia yao hii, bado utaendelea kuwaona wakija kila mara. Ukimpunguzia bei atasema ni mbinu ya kumvuta umuibie, ukimweleza ubora wa bidhaa atakuambia unamrubuni ili anunue, ukimwambia bei za vitu zimepanda atakuambia unamdanganya…n.k. Wateja hawa kamwe huwez kuwaridhisha kwani kila mara huona kuwa mfanyabiashara si mwaminifu/anapata faida kubwa sana kwa ujanja ujanja.Kwa kuwa wateja hawa hupenda kuongea sana, ni muhimu ukaangalia jins ya kutumia hekima kuwajibu na kuwahudumia ili wasije wakaeneza sifa mbaya kwa wateja wengine.

8. Wateja wasiokuwa na mpango wa manunuzi

Wateja hawa hufanya manunuzi ambayo hawakuyapanga awali; mara nyingi hufanya manunuzi kutokana na tamaa ya macho au ushawishi wa marafiki au muuzaji. Ikiwa wewe ni mfanyabiashara mwenye ushawishi na unayejua kunadi bidhaa zako vyema, ni rahisi sana kuwapata wateja wa aina hii kwani utaweza kuwashawishi wateja ambao hawakuwa na malengo ya kununua bidhaa zako wazinunue. 9.Wateja wanaotafuta ubora Wateja hawa hawatishiwi na bei wala hawapendi kuomba punguzo,wanachozingatia ni ubora wa bidhaa au huduma wanayoitaka.

Je, umewahi kujiuliza inakuwaje mtu anaacha kiatu cha ngozi cha Sh 50,000 na kwenda kununua kiatu cha ngozi cha Italia chenye thamani ya Sh 650,000? Hii ni kutokana na sababu kuwa mteja huyu anataka ubora wa bidhaa yake.Ikiwa unataka kuwapata wateja wa aina hii, basi zingatia kuweka bidhaa za bei tofautitofauti kwenye biashara yako. Kumbuka, bidhaa za bei ghali zinatakiwa kuwepo kwa uchache na baada ya kufanya tathimini kubwa kwani mzunguko wake ni mdogo sana kutokana na uchache wa wateja wake.

#Hitimisho Naamini umejifunza mengi kuhusu aina hizi 9 za wateja nilizozieleza katika makala hii. Bila shaka wateja ni watu muhimu sana, Je wewe uko kwenye kundi gani la wateja? Je wateja wako wengi wako kwenye kundi gani? Tafadhali andika maoni yako hapo chini kisha washirikishe wengine makala hii

Ahsante

Imeandikwa na Fortune King kutoka twitter.

0 replies

Leave a Reply

Want to join the discussion?
Feel free to contribute!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *